Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Zaidi ya wanajeshi 240 wa majini kutoka nchini Uturuki wamewasili humu nchini kupitia Bandari ya Mombasa ili kusaidia kuimarisha usalama katika bahari hindi ya Pwani Kenya.

Akiongea na wanahabari wakati wa uzinduzi rasmi wa meli ya jeshi la wanamaji kutoka Uturuki katika Bandari ya Mombasa siku ya Jumanne, Balozi wa Uturiki nchini Kenya Deniz Eke amesema kwamba wanajeshi hao watashirikiana wa wanajeshi wa majini wa Kenya katika kuwakabili maharamia.

Eke amesema kwamba jeshi hilo limezuru humu nchini na meli yao ya kijeshi ya zaidi ya mita 138 iliyobeba ndege ya kivita na vifaa vingine vya kisasa vya kivita kukabiliana na maharamia ili kudhibiti kuenea kwa maharamia katika mipaka ya Kenya na Somalia katika bahari hindi ya pwani ya Kenya.

Kulingana na Eke, hatua ya kuwasili kwa wanajeshi hao humu nchini iliafikiwa na serikali ya Kenya na Uturuki kupitia muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kushinikiza juhudi za kuimarisha usalama wa kimataifa katika baharini.

"Wanejshi wetu wamewasili humu nchini kushirikiana na wanajeshi wa maji wa kenya katika juhudi za kuimarisha usalama wa baharini na kukabalina na maharamia katika bahari hindi ya pwani ya Kenya kutokana na kushuhudiwa kwa meli nyingi zikitekwa nyara na maharamia," alisema Balozi Eke.

Amesema kwamba wanajeshi hao watasalia humu nchini kwa muda wa mwezi mmoja wakibadilishana mawazo na mbinu za kukabiliana na wahalifu na maharamia ili kuona kwamba idadi ya kutekwa nyara meli inapungua.

Hata hivyo uzinduzi huo umeshuhudiwa na viongozi wa serikali kuu na zile za kaunti ikiwemo Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho, Seneta wa kaunti hiyo Hassan Omar Sarai, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti Bollo, Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi na viongozi wengine.