Shirika la utetezi wa haki za kibanadamu la Haki Afrika linaishinikiza serikali kuzidisha kuweka amani nchini Somalia ili kuhakisha kuwa usalama katika mipaka ya Kenya na Somalia na maeneo mengine nchini unaimarishwa.
Afisa mratibu wa mipango katika shirika hilo Francis Auma Gamba amesema kuwa serikali haifai kutoa wanajeshi hao nchini Somalia kwani hatua hiyo itadhihirisha wazi kuwa serikali imeshindwa kukabiliana na magaidi na itakuwa tishio kubwa kwa taifa hilo dhidi ya magaidi.
Akiongea na wanahabari katika afisi za shirika hilo, Gamba amesema kuwa wananchi na serikali wako na imani na wanajeshi wa Kenya KDF na serikali iko macho kuhakikisha kuwa usalama wa taifa hili unaimarishwa.
"Tunaiomba serikali kutowaondoa wanajeshi wa Kenya KDF nchini Somalia kwa minajili ya usalama wa wananchi hadi taifa la Somalia na mataifa mengine kuwa na usalama kwa sababu hatua hiyo itadhihirisha wazi kuwa jeshi la Kenya limeogopa na ndio magaidi watatuvamia zaidi," alisema Gamba.
Gamba amewataka Wakenya kuungana na kuzidi kudumisha amani hasa wakati ambapo taifa la Kenya linapoomboleza kwa kuwapoteza wanajeshi wa Kenya KDF katika shambulizi la uvamizi lililotekelezwa na wanamgambo wa Alshabab nchini Somalia.
Kuali ya mwanaharakati huyo imejiri siku mbili tu baada ya baadhi ya mashirika ya kijamii ikiwemo shirika la Muhuri kupendekeza serikali kuwaondoa wanajeshi wa Kenya KDF nchini Somalia.