Wanakandarasi wanaojenga Maili Sita wameonywa dhidi ya kutumia bidhaa duni za ujenzi.
Afisa wa ukaguzi wa majengo katika kaunti ya Nakuru Peter Oduor amesema kuwa baadhi ya wanakandarasi na wajenzi wanatumia vyuma duni wakati wanapojenga.
Akizungumza alipoongoza shughuli ya kuyakagua majengo mtaani mailisita siku ya jumapili, Oduor alisema kuwa serikali ya kaunti italazimika kuyabomoa majengo yote yanayojengwa kwa kutumia vifaa duni.
Alisema hatua hiyo itachukuliwa ili kuepusha maafa ya majengo kuporomoka na kuwaua watu wasiokuwa na hatia.
“Kuna majengo mengi sana yanajengwa katika eneo hili lakini mengi utapata yanajengwa kutumia bidhaa duni sana na tunatoa onyo kwa wanakandarasi wote na wajenzi wahakkikishe kuwa wanatumia vifaa ambavyo vimeidhinishwa na vienye ubora wa juu,” alisema Oduor.
“Tutalazimika kuyabomoa baadhi ya majengo na kusimamisha ujenzi wa mengine kama njia ya kuepesha hatari ya kuporomoka kwa majengo,” alisema.
Aliwataka wajenzi, wamiliki wa majengo na wanakandarasi kuweka mbele maslahi ya wananchi ama watumizi wa majengo hayo kila mara wnapojenga.
“Kama watu watawacha tama ya pesa na kuweka maslahi ya raia mbele basi hii mambo ya kujenga majumba haraka haraka haitakuwa na ila mtu atakuwa salama,” aliongeza.
Afisa huyo alisema kuwa serikali ya kaunti itaendesha ukaguzi wa majumba katika kila mtaa ili kuhakikisha yako salama kutumia na binadamu.