Wito umetolewa kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu utendakazi duni wa maafisa wa polisi wa ngazi za chini, kama hatua ya kutathmni utendaji kazi wao.
Akitoa kauli hiyo siku ya Jumapili, kamishina wa tume ya huduma kwa polisi Murshid Abdalla Mzee alisisitiza kuwa taarifa hizo zitatumika katika ukaguzi wa maafisa hao kuhusu utendakazi wao.
Katika mahojiano ya kipekee na mwanahabri huyu, Murshid alisema mwananchi anaweza kutoa taarifa hizo kupitia vyama vya kutetea haki za kibinadamu ili kumaliza ufisadi unaoendelea katika idara zote za usalama humu nchini.
Aidha, alisema idara ya polisi imeimarika katika kutekeleza wajibu wao, ila wachache ndio wasiowajibika.
"Polisi wamebadilika pakubwa, ila kuna wachache tu ndio bado, ni mhimu kushirikiana na wananchi ili kupata habari inayoweza kusaidia kuimarisha usalama," alisema Murshid.
Vile vile aliongeza kuwa tume hiyo inajizatiti kukabiliana na visa vya ufisadi katika idara ya polisi nchini.