Wananchi sasa wamehimizwa kuwakagua viongozi kabla kuwapigia kura ili kuhakikisha kuwa wanachagua viongozi wenye maadili mema na wenye rekodi za kutenda kazi badala ya kuwachagua kwa msingi wa ukabila na chama.
Kwenye maombi yake kwa taifa, askofu mkuu wa kanisa la Kikatoliki jimbo la Mombasa Martin Kivuva, wakati umefika kwa taifa kuongozwa na viongozi watakao hubiri utangamano, undugu, uridhiano na kusamehana badala ya wale wanayoyatoa matamshi yanayoweza kuchochea na kusababisha mgawanyiko.
Aidha, Kivuva aliwahimiza waumini na wahubiri kuwa katika mstari wa mbele kutangaza uwiano na umoja wakati huu ambapo joto la kisiasa la mwaka 2017 limeanza kutanda katika sehemu mbalimbali nchini.
‘’Sisi kama viongozi wa kanisa lazima tuonyeshe kwa mfano, tuwe wenye kuongoza kwa vitendo, tuweze kuhubiri amani miongoni mwetu. Tupendane na tuwasaidie wasiojiweza katika jamii,’’ alisema Kivuva.
Kiongozi huyo wa kidini alikuwa akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi katika kanisa la Kikatoliki lililoko eneo la Tudor, ikiwa ni siku ya tatu ya maombi kwa taifa maarufu kama siku arobaini ya maombi inayolenga kuliombea taifa kutokana na changamoto mbalimbali zinazolikabili.