Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wananchi wa eneo la Nakuru wameombwa kuwa waangalifu na matumizi ya mafuta katika shughuli yao ya kila siku ili kuzuia visa vya kuzuka kwa moto kutokana na bidhaa hiyo hatari.

Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la viwanda la Nakuru ambapo moto ulizuka na kuteketeza kiwanda kimoja, Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua ameelezea kuwa mafuta ambayo huhifadhiwa mara nyingi huwa na hatari kwa maisha ya wananchi hivyo basi tahadhari inapaswa kuzingatiwa kwa wale wanohusika na bidhaa hiyo.

"Watu ambao wanahusika na uuzaji au usafirishaji wa mafuta wanapaswa kuwa waangalifu zaidi katika kushughulikia bidhaa hiyo na lazima wawe na utaalam wa hali ya juu ya kushughulika ma bidhaa hiyo. Mafuta ni bidhaa hatari na inaweza kusababisha maafa mengi na watu kupoteza mamilioni ya mali," Mbugua alisema.

Mbugua ambaye alikuwa akitalii eneo hilo ambalo kulizuka moto siku ya Jumatano mchana pia alihakikishia wenyeji wa eneo hilo kuwa serikali yake itakuwa makini kukabiliana na visa kama hivyo pindi vitapotokea.

‘Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila kaunti ndogo ya Nakuru imepewa magari ya kuzima moto ili kukabiliana na visa hatari kama hivi haraka iwezekanavyo. Tutazidi kutumikia wananchi ili kuhakikisha kila mmoja anapata maisha bora na usalama.’ Mbugua alielezea.

Moto huo umeripotiwa kuangamiza idadi ya mali isiyojulikana katika kiwanda hicho cha magodoro.