Huenda watu walio na mazoea ya kuajiri watoto kufanya kazi za sulubu katika kata ya Keera wakakabiliwa vikali kisheria.
Haya ni kulingana na chifu wa eneo hilo John Oire aliyekuwa akiwahutubia wanahabari kwenye hafla moja katika eneo la Nyaisa siku ya Ijumaa, aliposema kuwa kamwe hatovumilia tabia za aina hiyo.
"Kuna watu ambao bado wangali na mazoea ya kuwaajiri watoto ili kuwafanyia kazi za sulubu nyumbani, ila wacha wafahamu kuwa watoto hao wana haki ya kupata elimu na kamwe afisi yangu haitoketi na kuona haki zao zikihujumiwa na ndio maana yeyote atakaye patikana na hatia hiyo sharti akabiliane na sheria," alisema Oire.
Akizungumzia swala la kuwapa motisha wanafunzi ili kunawiri kwenye masomo, Oire alisema kuwa yafaa wanafunzi wazawadiwe kila mara wanapofanya vyema darasani.
"Ili mtu yeyote afanye vyema zaidi katika shughuli yeyote ile sharti azawadiwe, na ndio maana naona ni kheri wanafunzi wazawadiwe kila mara wanapoimarika masomoni na wala sio tu kwenye hafla kama hii," aliongezea Oire.
Picha: Chifu wa eneo la Keera John Oire. Amewapa onyo wale wote wanaowaajiri watoto katika eneo hilo kuwa watakabiliwa na sheria vikali. Wmaina/Hivisasa.com