Wakazi wanaoishi katika ufuo wa Mto Athi wameombwa kuhama ili kuepuka majanga yanayotokana na mto huo kufurika.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu kwa njia ya simu siku ya Jumatatu, OCPD wa Matungulu, Joseph Cheshire alisema kuwa mto huo hujaa maji na kuvunja kingo msimu wa mvua kubwa na huenda ukaleta madhara.
Aliwaomba wanaoishi kando ya mto huo kuhama kabla ya mto huo kuvunja kingo zake ili kuepuka majanga.
"Nimepata habari kuwa kuna watu ambao bado hawajahamisha makao yao na hiyo ni hatari mno kwani huenda mto huo ukavunja kingo na kuleta madhara kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa. Ningependa Kuwatahadharisha wakazi kabla ya hatari kutokea,” alisema Cheshire.
Aidha, afisa huyo aliwaonya wakazi dhidi ya kusubiri hadi pale majanga yatakapotokea ili kuomba msaada kutoka kwa serikali.
"Sio vyema kungoja hadi pale madhara yamepatikana ndio muanze kutafuta suluhu ilhali mlitahadharishwa mapema,” alisema Cheshire.