Wananchi wanaoishi karibu na Ziwa Victoria wameonywa dhidi ya kuchafua ziwa hilo, hasa kupitia kuosha magari ziwani humo.
Inspekta wa Maamlaka ya usalama baharini (KMA), tawi la Kisumu Jeremiah Onyango amesema kuwa kuchafuliwa kwa Ziwa Victoria huenda kukasababisha madhara kwa wananchi wanaotumia maji ya ziwa hilo na wanyama wanaoishi humo.
Akizungumza jijini Kisumu mnamo Jumatatu, Onyango alisema kuwa ni hatia kwa mtu yoyote kuosha magari Ziwani Victoria, akisema kuwa ni lazima tabia hiyo ikome.
“Maji ya Ziwa Victoria hayalipishwi. Una uhuru wa kufanya chochote na maji hayo lakini sio kulichafua Ziwa,” alisema Onyango.
Aliwakemea wale wanaomwaga maji taka Ziwani Victoria, akionya kuwa watakabiliwa vikali kisheria, na kisha kutoa wito kwa wadau wote katika sekta ya mazingira kushirikiana kuhakikisha kuwa ziwa hilo linasalia safi.
Ziwa Victoria limekuwa likichafuliwa hasa na vijana wanaofanya kazi ya kuosha magari kwenye fuo mbali mbali za ziwa, hasa ufuo wa Lwang’ni mjini humo.
Vile vile, uchafu unaotokana na mabaki ya ugemaji wa pombe haramu mtaani Obunga jijini Kisumu huelekezwa ziwani humo, hivyo kuhatarisha maisha ya watu wanaotumia maji ya ziwa hilo.
Ziwa Victoria limetanda katika Kaunti za Kisumu, Homabay, Migori na Busia humu nchini, huku maji ya ziwa hilo yakutumiwa na maelfu ya watu kila siku.