Idara ya usajili wa watu katika ukanda wa pwani imewaonya wanaowaitisha mlungula kwa wananchi ili kuwasaidia kupata vyeti vya kitaifa kuwa watakabiliwa kisheria.
Kulingana na msajili mkuu wa watu eneo la Pwani Aggrey Masai, kuna baadhi ya mawakala wanaotumia fursa hiyo kuwalaghai wananchi hasa katika maeneo ya Lunga lunga, Msambweni na Mwareni kaunti ya Kwale wakidai kuwa watawasaidia kupata vitambulisho vya kitaifa.
Akiongea na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Masai amesema kwamba maafisa wa idara hiyo wamo nyanjani kuwachunguza wanaoendeleza ulaghai huo ili kuwatia nguvuni na kufunguliwa mashtaka na akasema kwamba vyeti hivyo vya kitaifa vinatolewa kwa wananchi bila malipo.
Masai aidha amesema kwamba idara hiyo iko na uwezo wa kuwapima wananchi na kutambua miaka yao na akawataka kujiepusha na watu kama hao walaghai kwani kinachohitaji na idara hiyo ni vyeti vya mzazi iwapo mtu anahitaji kitambulisho.
"Tunawaonya vikali wanaowalaghai wananchi kwa kuwatisha pesa ili wawasaidie kupata vitambulisho kuwa watakabilia kisheria na tunawataka wananchi wafahamu kuwa vyeti hiyo vinatolewa bure bila malipo," alisema Masai.
Kauli ya afisa huyo mkuu wa idara ya usajili wa watu hapa pwani imejiri baada ya lalama kutoka kwa wananchi kuitishwa pesa na mawakala ili kupata vyeti hivyo muhimu vya kitaifa.