Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafanyibiashara na wamiliki wa makampuni wanaokwepa kulipa ushuru katika Kaunti ya Nakuru huenda wakanyanganywa leseni za kuhudumu.

Mkuu wa Idara ya fedha katika Kaunti ya Nakuru, Anne Njenga, amesema kuwa kuna baadhi ya wafanyibiashara wanaokwepa kulipa kodi kwa kushirikiana na maafisa walaghai wa serikali ya kaunti.

Akihutubu afisini mwake siku ya Jumanne, Njenga alisema kuwa afisi yake imeanza utaratibu wa kuyatambua makampuni na biashara zinazokwepa kulipa kodi na watawaandikia barua ya kulalama.

Mkuu huyo wa idara alisema kuwa ukwepaji kulipa kodi unaisababishia serikali ya kaunti hasara ya mamilioni ya pesa.

“Kuna baadhi ya watu ambao wana tabia ya kukwepa kulipa kodi kwa serikali na wanafanya hivyo kwa kushirikiana na baadhi ya maafisa wetu. Tunawapa onyo kwamba tumeanza uchunguzi wa kuwatambua na wasipobadilika tutawataja hadharani na kuchukua leseni zao,” alisema Njenga.

Aliongeza, “Pia tunawaonya maafisa wa serikali ya kaunti ambao wanashirikiana na wafanyibiashara kuibia serikali kuwa siku zao zimehesabika na tutawanasa.”

Bi Njenga alisema kuwa itakuwa vigumu kwa serikali ya kaunti kutekeleza ahadi zake na kutoa huduma kwa umma iwapo watu watakwepa kulipa kodi.

Aliwahimiza wafanyibiashara kuwa wazalendo na kuipenda kaunti yao kwa kutekeleza jukumu la kulipa kodi.