Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wanasiasa wanaoendeleza kampeni za uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Malindi wameonywa dhidi ya kuwahadaa wakazi wa eneo hilo ili kuwarai wawapigie kura.

Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani Nelson Marwa alisema kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wanaozuru nyumba hadi nyumba nyakati za usiku na kuwasajili wakaazi kisha kuwahonga na akasisitiza kwamba njama hiyo iwapo ni ya wizi wa kura kamwe haitafulu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Marwa aliwahakikishia wakaazi wa eneo la Malindi usalama wa kutosha wakati wa kampeni hizo, na wakati wa uchaguzi siku ya Jumatatu juma lijalo na akawaondolea hofu ya kuzuka kwa vurugu.

Wakati huo huo, Marwa aliwatadharisha wanasiasa wanaoendeleza kampeni hizo dhidi ya kutoa matamshi ya uchochezi na yanayolenga kuwagawanya wakaazi katika eneo bunge hilo la Malindi.

"Serikali iko macho kuwakabili wale wote wanatoa siasa za chuki na uchochezi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Malindi ili kuona kuwa shughuli hiyo inafanywa kwa amani na uwazi, hatutaki kushuhudia ghasia, na atakayepatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Marwa.

Hata hivyo, Marwa amewahimiza wakaazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya Jumatatu tarehe 7 Mwezi Machi ili kumchagua kiongozi wao wanayemtaka baada ya aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo Dan Kazungu kukabidhiwa Wizara ya madini.

Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani Nelson Marwa. Amewataka viongozi wa kisiasa wanaondeleza kampeni za uchaguzi mdogo Malindi kuzifanya kwa amani.