Viongozi wanaolenga kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao wameonywa dhidi ya kutoa matamshi ya chuki, ambayo huenda yakawachochea Wakenya.
Akizungumza kwenye shughuli ya kutoa fedha za ufadhili wa masomo katika uwanja wa Mkarafuu viungani mwa mji wa Nakuru siku ya Ijumaa, Kamishna wa Kaunti ndogo ya Nakuru Thomas Sankei, alisema kuwa yeyote atakayepatikana na kosa hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Sankei alisisitiza kwamba maafisa wote wa polisi tayari wameagizwa kuchukua hatua hiyo.
Kulingana naye, Nakuru ni mji ulio na makabila yote na hivyo ukabila unafaa kutupiliwa mbali.
“Kila mtu ana uhuru wa kuunga mkono chama chochote kile na kuwania kiti chochote bila kushurutishwa, kwani Kenya inazingatia mfumo wa demokrasia katika uchaguzi,” alisema Sankei.
Aliyekuwa diwani katika wadi ya Kapkures kwenye kaunti ya Nakuru Joseph Ngetich, ambaye pia alikuwa miogoni mwa waliojumuika kwenye shughuli hiyo, aliwataka machifu kufanya mikutano ya mara kwa mara na wakaazi, ili kuwasilisha taarifa mbalimbali pamoja na kuwahimiza wakaazi kuishi kwa amani.
Aidha, aliwataka wakaazi wa Kaunti ya Nakuru kudumisha amani wakati wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.
Alisisitiza kwamba machifu hawafai kusubiri hadi mambo yawe mabaya, bali wanafaa kuchukua hatua kutatua changamoto zinazowakumba wakaazi wa maeneo yao kwanza.
Takriban shilingi milioni kumi na tano zilitolewa kufadhili masomo katika shule hizo na hazina ya eneo bunge la Nakuru Magharibi.