Wanasiasa wa eneo la Pwani wamehimizwa kukoma kupiga siasa za mapema na badala yake wajihusishe na shughuli za ujenzi wa taifa pamoja na kuitekeleza miradi ya maendeleo kwa wakazi. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumamosi, afisa mratibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika, Franics Gamba aliwataja wanasiasa hao kama wanaojali maslahi yao ya kibinafsi badala ya wananchi waliowachagua.

Gamba alisema ni jambo la kushangaza kuwaona wanasiasa wa Pwani wakijitosa katika siasa na kulumbana hadharani ilhali tume huru ya mipaka na uchaguzi nchini haijatangaza tarehe ya uchaguzi.

''IEBC haijatangaza tarehere ya uchaguzi wa 2017, sasa unashindwa hawa wanasiasa wetu wana haraka gani,'' alisema Gambo.

Aidha, aliwataka wanasiasa hao kuwaelezea wananchi yale walioyafanya kipindi walichokua uongozini kabla kutaka kupigiwa kura tena kwa hatamu nyingine. 

''Tunataka watuambie nimefanya hiki na kile na ninalenga kuhitimisha hili na lile mkinichagua tena,'' aliongeza.

Mwanaharakati huyo vilevile aliwahimiza wakazi wa Pwani kujitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura pindi shughuli hiyo itakapoanza, kwani ndiyo njia ya pekee itakayowapa nguvu ya kuwachagua viongozi wawajibikaji na wenye maadili mema.

Siku za hivi majuzi wanasiasa wengi wa Pwani wameonekana kuanza siasa za mapema huku wengine wao wakitangaza kuvihama vyama vyao na kujiunga vyama vingine kuelekea uchaguzi wa 2017 hususan wakati wa ziara ya Rais Kenyatta mjini Mombasa.