Diwani wa zamani katika eneo la Gesima Jane Nyakong'o amewaonya vikali wanasiasa ambao wamekuwa wakimshtumu mkewe gavana wa kaunti ya Nyamira Bi. Naomi Nyagarama kwa madai ya matumizi mabaya ya raslimali za umma.
Akiwaongoza wakazi wa Gesima kumtetea mkewe gavana, Nyakong'o alisema kuwa nia ya wanasiasa wa aina hiyo ni kuathiri miradi ya maendeleo inayotekelezwa na BNyagarama.
“Ni vibaya kwa wanasiasa wengine kudai kwamba Nyagarama anatumiwa ili kuvuja rasmali za umma kwa kuwa sasa wasichana wetu wanaweza kaa shuleni na baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wameacha shule kwa sababu ya kuathirika na funza wamerejelea masomo yao kama kawaida,” alisema Nyakang’o.
Mwanasiasa Jerusa Momanyi aliongeza kusema kuwa shughuli anazo ziendesha mkewe Nyagarama ni halali, na akawasuta vikali wapinzani wake akisema kuwa ni vizingiti vya maendeleo.
“Wanasiasa hao wanaopinga maendeleo hawataki afanye miradi anayoitaka, na iwapo wanataka kusaidia kwenye miradi hiyo tutamwomba Nyagarama awaruhusu kutoa usaidizi,” alisema Momanyi.
Haya yalijiri baada ya mshauri wa kifedha wa benki ya dunia tawi la Kenya Charles Mochama kunukuliwa huko Rigoma alipokuwa akiwahutubia wakazi akisema kuwa afisi ya gavana inamtumia Bi Nyagarama kuvuja pesa za umma.