Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la Kibiashara na Viwanda nchini yaani National Chambers of Commerce and Industry limewashinikiza viongozi wa kisiasa kuwepo tafauti zao za kisiasa kando na kuwatekelezea wakenya maendeleo.

Mwenyekiti wa Shirika hilo Kaunti ya Mombasa James Mureu amesema kuwa malumbano ya kisiasa ya mara kwa mara huenda yakasambaratisha shughuli za kibiashara ambazo tayari zimeanza kuimarika kote nchini baada ya kukumbwa na changamoto za kiusalama.

Akiongea na wanahabari katika afisi za Shirika hilo mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mureu alisema kuwa jukumu la viongozi hao ni kuhakikisha kuwa maswala ya kimaendeleo na biashara nchini yanatekelezwa na kuweka tofauti zao kando kwani wakati huu sio msimu wa kisiasa.

Amesema kuwa kuendelea kushuhudiwa kwa malumbano ya kisiasa ni hatari zaidi kwa vijana kwani wengine wao hujikuta katika maswala ya itikadi kali na kuvuruga usalama wa taifa hili na kusambaratisha uchumi wa nchi.

"Kushuhudiwa kwa viongozi wa kisiasa wakilumbana hadhara kila uchao huenda kukasababisha vijana kujikuta katika makundi ya itakadi kali na kuvuruga usalama, hali ambayo ni hatari zaidi kwani husambaratisha uchumi na biashara nchini," alieza Mureu.

Kauli ya Mureu imejiri siku mbili tu baada ya viongozi wa kisiasa kushuhudiwa wakilumbana hadharani katika hafla ya kutoa hati miliki za ardhi kwa wakazi wa Shamba la Waitiki iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto pamoja na viongozi wengine serikali.