Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi wa kisiasa katika eneo la pwani wamehimizwa kusitisha siasa na matamshi ya uchochezi yanayolenga kuwagawanya wakenya kwa misingi ya kikabila, kidini na kisiasa.

Akiongea na wanahabari katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kiongozi wa Vijana katika eneo hilo Maxwell Masai alisema kuwa iwapo viongozi watazidi kulumbana hadharani na kuwachochea wakenya basi eneo hilo litaangamizwa.

Masai alidai kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanawachochea vijana kuzua rabsha na kuvuruga usalama wa eneo hilo kwa manufaa yao binafsi, jambo ambalo alilikashifu.

"Kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwachochea wakaazi wa eneo hili kuzua vurugu kwa misingi ya kikabila na chuki. Sisi kama vijana hatuwezi kukubaliana nalo na tunawahimiza maafisa wa usalama kuwachunguza na kuwachukulia hatua," Masai alisema.

Kiongozi huyo amewahimizwa maafisa wa usalama na makamisha wa tume ya kukabiliana na matamshi ya chuki wawachukulia hatua wanasiasa hao.