Mwaniaji wa ubunge katika eneo bunge la Borabu Nyandoro Kambi amejitokeza kuwahimiza wanasiasa kutoingisha siasa suala la usajili wa wapiga kura linaloendeshwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kote nchini.
Akihutubia wakazi wa Tinderet kwenye zoezi la kuwahamasisha wananchi kuhusiana na umhimu wa kujisajili kama wapiga kura katika shule ya msingi ya Tinderet, Kambi aliwaomba wanasiasa kuwasilisha lalama zao kuhusiana na zoezi hilo la usajili wa wapiga kura badala ya kulalama kwenye mikutano.
"Ningependa kuwaambia wanasiasa wenzangu kutoingisha siasa suala hili la usajili wa wapiga kura kwa maana iwapo wana kitu wanachoona kuwa sio kizuri, sharti wawasilishe lalama zao kwa maafisa wa tume ya IEBC badala ya kulalama kwenye mikutano ya hadhara," alisema Kambi.
Kambi aidha aliwahimiza wanasiasa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kusajiliwa kama wapiga kura, huku akiitaka tume ya IEBC kutokubali kuingililiwa na wanasiasa.
"Kama wanasiasa twafaa kusaidia tume ya uchaguzi nchini kufanikisha zoezi lake kwa kuhamasisha wananchi kujitokeza ili kusajiliwa kama wapiga kura, na yafaa tume hiyo isikubali kamwe kuingililiwa kisiasa na matamshi ya baadhi ya wanasiasa," aliongezea Kambi.