Changamoto imetolewa kwa kila mmoja katika jamii kushirikiana katika vita dhidi ya ugonjwa wa saratani nchini.
Kulingana na afisa katika hospitali ya Hospice jijini Kisumu Rose Okwara, hatua ya kupigana na saratani ya shingo ya kizazi ‘cervical Cancer' haipaswi kuachiwa wanawake pekee, na hata wanaume wanapaswa kushiriki juhudi za kufaulisha vita dhidi ya saratani.
''Ni vyema kila mmoja afike katika vituo vya kiafya ili wapate kujua afya yao ndiposa tuweze kuwasaidia mapema endapo watapatikana kuwa na saratani, ukweli ni kuwa ikigundulika mapema saratani ina tiba,'' a;isisitiza Okwara.
Katika mahojiano ya kipekee afisa katika shirika la Tumaini la Maisha Health Services Lameck Oyoo, ametoa wito kwa wanaume wenye umri wa miaka 45 kufika katika vituo vya matibabu kupimwa kiwango cha antijeni aina ya Prostrate Specific Antigen (PSA) ili kusaidia kukabili saratani ya shingo ya uzazi.
"Yeyote ambaye angependa kujua mwelekeo kuhusu saratani na usaidizi anaweza akawasiliana na wadau katika sekta ya afya Nairobi na watapewa mwelekeo wa ni vipi anaweza akapata ushauri nasaha na msaada zaidi," alisema Oyoo.
Esther Okech, wakili katika shirika la KEFIADO na ambaye pia ni mmoja wa walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya saratani, aidha alisisitiza kuwa ni vyema kila mmoja kuhakikisha anafanyiwa uchunguzi wa saratani kila baada ya mda flani ili kufanikisha uwezo wa kuutibu ukiwa ungali katika kiwango kidogo.
Kuhusu matibabu ya saratani, wataalamu hao wametoa wito kwa jamii kutozingatia dhana kuwa maradhi ya saratani ni tiketi ya kifo na kusisitiza kuwa hatua za kwanza za saratani zinatibika.