Viongozi wanawake katika bunge la Kaunti ya Mombasa wamesema kuwa wanawake mjini Mombasa na Pwani kwa jumla wamekuwa wakiogopa kujihusiha katika uongozi, huku wakiamini kwamba siasa ni za wanaume peke yake.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, mwakilishi wa Wadi ya Magogoni, eneo la Kisauni Bi Zainabu Omar, alisema kuwa katika uchaguzi uliopita, wanawake wa Mombasa waliojitokeza kugombea viti mbalimbali walikuwa wachache mno licha ya kupewa fursa hiyo.
“Wakati huu ambapo tunaathimisha siku ya akina mama, mimi nasema ya kwamba mwanamke pia ni kiongozi na tuache imani kwamba wanaume ndio kila kitu katika jamii,” alisema Bi Omar.
Wakati huo huo, Omar alieleza masikitiko yake kwamba ni wanawake watatu tu peke yake waliochaguliwa katika bunge hilo kwenye uchaguzi uliopita, huku wengi wao wakiteuliwa.
Mbunge mteule katika bunge hilo Bi Zainabu Ali alisema kwamba wanawake wamekuwa wakipata ushindani mkubwa kutoka kwa wenzao wanaume.
Alisema kuwa mara nyingi wanaume huwa wanapinga hoja wanazowasilisha bungeni lakini wao hujikakamua na kukabili changamoto hiyo.
“Tukitoa hoja bungeni lazima watatupinga lakini tunajitahidi mpaka mwishowe inapita. Hizo ni baadhi ya changamoto tunazopitia kama wanawake lakini hatuwezi kusema tutarudi nyuma,” alisema Ali.
Alisema kuwa viongozi akina mama pia hupitia changamoto ya kushughulikia maswala ya uongozi na familia kwa pamoja.
Wawakilishi katika bunge la Mombasa sasa wamesema kuwa wataendeleza uhamasisho kwa jamii pamoja na shuleni ili kuwaelimisha wasichana hasa katika vyuo vikuu kujitosa katika uongozi ili kubadilisha maisha ya akina mama.
Siku ya wanawake ulimwenguni husherehekewa tarehe 8, mwezi Machi kila mwaka, lengo kuu ikiwa ni kuangazia mambo anayopitia mwanamke pamoja na changamoto zake.
Katika sherehe za mwaka huu, wananchi wa Mombasa watajumuika pamoja katika uwanja wa Tononoka ambapo Mwakilishi wa akina mama katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko ataongoza wakaazi katika hafla hiyo.