Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mratibu wa masuala ya jinsia katika shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika, Bi Salma Hemed, amedai kuwa wanawake walitengwa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi uliofanyika siku ya Jumatatu.

Akizungumza mjini Malindi siku ya Jumatatu, afisa huyo mtetezi wa haki za wanawake na watoto aliitaja hatua ya vyama vya kisiasa nchini kuwaunga mkono wanaume pekee katika uchaguzi huo kama ubaguzi wa kijinsia.

“Uchaguzi wa Malindi ni mfano tu wa namna wanawake tunavyosahaulika katika jamii. Iweje hakuna hata mwanamke mmoja aliyesimama katika uchaguzi huu?” aliuliza Hemed.

Hemed alieleza kukerwa na kukosekana kwa wanawake kugombea kiti hicho, na kuwataka wanawake kutoka ukanda wa Pwani kujisali kwa wingi kama wapiga kura kabla ya zoezi hilo kukamilika.

Alisema kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee itakayowapa nguvu ya kumsimamisha mmoja wao.

Aidha, mtetezi huyo wa haki za binadamu aliwahimizi wanawake kutoka eneo la Pwani kuziwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao, ili waweze kuzitetea na kupata haki zao za kidemokrasia.

Uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi uliwavutia wanawaume pekee huku upinzani mkali ukishuhudiwa kati ya Philip Charo wa Jubilee na Willy Mtengo wa ODM.