Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi mkuu wa sekta ya afya katika kaunti ya Kisii amewashauri akina mama kufika katika hospitali mara moja kwa mwaka ili kupimwa ugonjwa wa saratani.

Wito huo ulitolewa baada ya kubainika kuwa saratani ya mfuko wa uzazi kwa akina mama ndio inaongoza kwa asilimia kubwa ikilinganshwa na saratani za aina zingine.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika hospitali ya rufaa na mafunzo iliyoko mjini Kisii wakati wa kuadhimisha siku ya saratani ulimwenguni,  mkurugenzi wa afya katika kaunti ya Kisii Geoffrey Ontomu aliomba akina mama kufika hospitalini kupimwa ugonjwa wa saratani mara moja kwa mwaka.

Kulingana na Ontomu, mtu anapogunduliwa kuwa ameathirika na ugonjwa wa saratani aina yoyote huwa rahisi kutibiwa kabla ya kuenea mwilini.

“Sarani ni ugonjwa ambao umekuwa ugonjwa wa tatu kwa mauaji lazima sisi zote tujitolee kupambana na ugonjwa huo,” alisema Ontomu.

“Naomba akina mama wote kufika katika hospitali yetu ya rufaa hapa Kisii kupimwa saratani mara moja kwa mwaka ili mtu anapopatikana iwe rahisi kutibu,” aliongezea Ontomu.

Aidha, Ontomu alisema kulingana na uchunguzi waliofanya katika kaunti ya Kisii, saratani ya mfuko wa uzazi kwa akina mama ndio inaongoza kwa asilimia 40, saratani ya moyo kwa asilimia 30, saratani ya kibofu kwa asilimia 10, saratani ya matiti kwa asilimia 7, huku ile ya tumbo ikiwa kwa asiliamia 6.