Wanawake katika Kaunti ya Kisii wameshauriwa kutotegemea wazee wao na kutafuta mbinu za kujiendeleza kimaisha.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wengi wa wanawake katika boma nyingi wamerudi nyuma zaidi kwani hutegemea wazee wao kila kitu, jambo ambalo limesemekana kuchangia hali ya umaskini.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Kisii, mwenyeki wa Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Kisii Bathseba Sanaya aliwashauri wanawake wa kaunti hiyo kutotegemea wazee wao kwani wanachangia umasikini katika familia nyingi, na kuwaomba kufanya biashara kujiendeleza.
Sanaya aliwahimiza wanawake kuchukua mikopo kutoka kwa mashirika mbalimbali ili kutumia kufanya biashara na kujiendeza na kupunguza hali ya umaskini katika Kaunti ya Kisii.
“Naomba kila mama katika kaunti yetu ya Kisii akuje apate mkopo ili atumie kufanya biashara na kujiendeleza kimaisha,” alisema Sanaya.
“Ile faida ambayo mama anapata kutoka kwa biashara zake, hakuna haja ya kuitumia, ni kuiweka ili ukuje kujisaidia nyakati zijazo. Uchunguzi unaonyesha umaskini umeongezeka Kisii kufuatia wanawake wengi hutegemea wazee wao kwa pesa na chakula, hawafikirii lingine la kufanya," alisema Sanaya.
Sanaya aliongezea kuwa ikiwa umaskini utapigiwa kwaheri, sharti kila mtu awe kijana, akina mama na wazee wajitolee kupambana na umaskini kwa kufanya kilimo pamoja na biashara ili umaskini kupungua.