Huku zikisalia siku mbili pekee kabla ya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi kufanyika, akina mama na vijana katika eneo hilo wahimizwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo mdogo.
Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa alisema kuwa wakati umefika sasa kwa wanawake kujitokeza na kumchagua kiongozi kwenye kujali maslahi ya wananchi mashinani ili kuona kwamba maswala ya maendeleo mashinani yanaangaziwa vyema.
Akionekana kumpigia debe mgombea wa kiti hicho kapitia chama cha ODM Willy Baraka Mtengo, Aisha aliwarai wanawake katika eneo bunge hili kuonyesha uiano na umoja na kumchagua kiongozi huyo huku akisema kuwa kiongozi huyo anajali maslahi ya wakaazi wote hadi mashinani.
Aisha alisema kuwa iwapo wakaazi wote watajitokeza na kumchagua kiongozi huyo moja kwa moja bila ya upinzani wowote basi watakuwa wameonyesha uzalendo pamoja na kuheshimu chama cha ODM kinachojali wakaazi wanyonge na kinachopigania haki za Wakenya wanaonyanyaswa.
“Tafadhali akina mama na vijana pamoja na wazee wetu kwa jumla siku ya Jumatatu ya uchaguzi mdogo wa eneo Malindi jitokezeni kwa wingi na mkamchague kijana wenu mwenye nia ya kufanya kazi na nyinyi na kuleta maendeleo ili kuelete uongozi bora na wakutetea wakaazi wetu,” alieleza Aisha siku ya Ijumaa katika mkutano wa akina mama.
Uchaguzi huo mdogo wa eneo Bunge la Malindi unatarajiwa kuwa na ushindani mkali baina ya chama cha ODM na Jubilee huku wafuasi wa Cord wakionekana mkpigia debe Willy Mtengo na Jubilee wakimpigia debe Philip Charo.