Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katibu Mkuu wa Muungano wa Kutetea Maslahi ya Wakulima wa Miwa nchini Francis Wangara, ameunga mkono mpango wa serikali wa kubinafsisha Kampuni tano za sukari nchini.

Akiwahubitia wanabahari jijini Kisumu siku ya Jumatano, Wangara alisema kuwa wanasiasa wasiruhusiwe kumiliki kampuni hizo chini ya mpango huo wa ubinafsishaji, akisema kuwa wanasiasa huenda wakachangia kudorora zaidi kwa viwanda vya sukari nchini.

“Tungependa kampuni hizi ziende kwenye mikono ya watu ambao watawajibika ipasavyo. Hatutaki ziende kwenye mikono ya wanasiasa au watu wanaofungamana na siasa,” alisema Wangara.

Aliwataka viongozi wa kisiasa katika maeneo kunakokuzwa miwa, kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wakulima wa miwa wananufaika na kilimo hicho.

Matamshi ya Wangara yalijiri saa chache baada ya Baraza la Magavana nchini, kuapa kuwanyima wanunuzi wapya leseni za kuendesha kampuni hizo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, baraza hilo lilisema kuwa matakwa ya magavana yamekiukwa na Tume ya Ubinafsishaji, kwani waliomba wananchi kupewa muda zaidi kutafuta hela za kununua hisa katika kampuni hizo tano, ambazo kwa sasa ziko chini ya serikali.

Magavana hao walisema kuwa lazima wananchi wawe na hisa kwenye viwanda hivyo, la sivyo shughuli zote za kuuza viwanda zisambaratike.

Mapema mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta aliamuru mpango wa uuzaji kampuni hizo kuharakishwa.

Kampuni hizo ni Sony, Miwani, Chemelil, Nzoia na Muhoroni.