Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi amewataka wananchi kuripoti maafisa wa polisi ambao watakuwa wakitekeleza jukumu lao la kuweka usama wakitumia magari yasiyo rasmi.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Mombasa siku ya Alhamisi, kamanda huyo alisema kuwa si haki hata kidogo maafisa wa usalama kutumia magari yasiyoruhusiwa kisheria kufanyia doria katika mitaa ya kaunti hiyo.
Aliwataka wakazi wote katika kaunti hiyo kutoa ripoti iwapo watawaona au watashikwa na maafisa wa polisi ambao watakuwa wakitumia magari yasiyo ya polisi.
Wanjohi alisema kuwa amepata malalamishi mengi kutoka kwa wakazi kuwa wengi wa waweka usalama wamekuwa wakiyatumia magari aina ya tuk tuk kuzungukia mitaani na kuwashika bila kuwaeleza sababu na kudai sheria hairuhusu polisi yeyote kutumia gari lolote mbali na ya polisi ambayo yameidhinishwa kisheria.
Alichukua muda huo kuwaonya wale watakaopatikana wavuruga usalama na kuchafua utaratibu wa sherehe kuwa watanaswa na kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuleta fujo.
Amesema haya wakati ambapo wakazi wa kaunti hiyo wamekuwa wakilalamikia kudhulumiwa na maafisa wa usalama wanapopiga doria mitaani.