Share news tips with us here at Hivisasa

Huku ulimwengu mzima unapojiandaa kufunga mwaka wa 2015 na kufungua mwaka mpya wa 2016, idara ya polisi katika Kaunti ya Mombasa imewakikishia usalama wakazi na kuwataka kushirikiana na maafisa wa usalama kutoa ripoti za visa vyovyote vya utovu wa usalama.

Akiongea jijini Mombasa, kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Francis Wanjohi alisema kuwa idara ya usalama inafanya kila juhudi kuona kuwa kila mkazi yuko katika hali nzuri na visa vya uhalifu vinadhibitiwa vilivyo.

Wanjohi alisema kuwa maafisa wake tayari wamekuwa wakipiga doria kila mtaa wa jiji hilo ili kukaba mipango yoyote ya wahalifu ambao mara nyingi alisema huchukua nafasi yao wakati kama huu wa shamra shamra za kusherehekea kufunga mwaka na kujihusisha katika visa vya wizi na kuwahangaisha wakazi.

Kamanda huyo aliwataka wakazi kuwa macho zaidi wanaposherehekea, na kuwaonya wale ambao watapatikana na hatia ya kujihusisha na visa kinyume na sheria kuea watatiwa mbaroni na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Amesema haya siku chache tu baada ya viongozi kutoka kaunti hiyo kulalama kuwa wakazi, hasa vijana wamekuwa wakidhulumiwa na baadhi ya maafisa wa polisi kwa kisingizio cha kuweka usalama, hali ambayo seneta wa kaunti hiyo aliitaja kuwa kinyume na haki za msingi za raia ambaye anatarajia kulindwa na polisi.