Wakazi wa Pwani wanapongeza hatua ya Vuguvugu la Mombasa Rebublican Congress, MRC la kuamua kujiunga na kujisajili kama wapiga kura.
Wakazi hao, wakiongozwa na Fatma Hussein, mkazi wa Majengo walisema na mwanahabari huyu siku ya Jumatano kuwa hatua hiyo italeta amani miongoni mwa wananchi hasa kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2017.
Fatma aliongeza kuwa yuko na imani kuwa hakutakuwa na vurugu wakati wa uchaguzi ikizingatiwa MRC imekubali kujiunga kama wapiga kura kwani ndio ilikuwa tishio kubwa kwa wakazi.
Itakumbukwa kuwa MRC ilijitokeza na kutangaza malengo ya kuwahimiza wenyeji wa Pwani kuishi kwa amani na kujiandikisha kuwa wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Wakiongea kwenye mkutano mmoja wa hadhara, wanachama hao, wakiongozwa na Rashid Mraja walisema kundi hilo litahakikisha kuwa wanachana wao watashiriki katika uchaguzi na pia kuwahimiza wakazi kujiandikisha.
Mraja alidokeza kuwa yuko tayari kutoa hamasisho kwa vijana wengine ambao walikuwa na mtazamo hasi hapo awali baada ya mawazo potovu ya kundi hilo na kusema kuwa sasa ni wakati wa kuja pamoja na kuungana kama jamii ili kusaidia kizazi na kuendeleza nchi.
“Tupo tayari, iwe ni kwenye mikutano ya hadhara, kwenye hafla za matanga kwenye makongamano ya harusi kuwahamasisha wenyeji umuhimu wa kuishi pamoja na umuhimu wa kujisajili kama mpiga kura kwenye eneo unaloishi,” alisema kiongozi huyo.