Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waraibu wa dawa za kulevya na pombe ambao wanahudumiwa katika kituo cha Haven Recovery mjini Eldoret wanataka bei ya pombe na vileo vingine kupandishwa.

Waraibu hao walisema hiyo itakuwa njia moja ya kulinda vijana dhidi ya kuzama katika uraibu wa dawa za kulevya.

Mbali na kupandisha bei ya bidhaa hiyo waraibu walitaka shirika la kupambani na uraibu wa dawa za kulevya na pombe Nacada kunoa makali yake dhidi ya vita hivyo.

Kwa mujibu wa waraibu hao ni kwamba kuingizwa nchini kwa mivinyo ya bei nafuu ni miongoni mwa maswala mengine ambayo yanachangia katika ongezeko la waraibu wa dawa za kulevya na pombe nchini.

Mmoja wa waraibu hao Walter Yegon alisema kuna haja ya sheria kuhusu udhibiti wa vileo kufanyiwa marekebisho na kupewa makali zaidi ili kubuni sharia kali zaidi za kukabiliana na dawa za kullevya.

“Kama sharia hii ingekuwa na nguvu hatungekuwa na vileo kalikali kutoka nje singekuwa nimeathiriwa hivi na uraibu wa pombe , nimepoteza mali yangu mbali na kutatiza familia yangu kwa sababu ya pombe singependa vijana wengine kupitia machungu ambayo nimeyapitia kwa sababu ya pombe,” alisema Yegon.

Yegon ambaye ni mhudumu wa afya katika eneo la Trans-Mara alisema hayo mjini Eldoret katika kituo cha Haven ambako anaendelea kupona kutokana na athari ya uraibu wa pombe maishani mwake.

Kituo hicho huhudumia takribani waraibu wa dawa za kulevya wapatao 1,000 kila mwaka.