Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Siku moja tu baada ya tume ya kudhibiti kawi nchini ERC kutangaza bei mpya za mafuta, wasafiri sasa wanawataka wenye magari kupunguza nauli.

Wasafiri waliozungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumatatu, wakiongozwa na Mzee Aba, walidai kukerwa na hatua ya wenye magari kupandisha nauli pindi bei za mafuta zinapopanda, lakini kudinda kupunguza nauli bei hizo zinapopunguzwa.

"Bei ya mafuta ikipanda wanapandisha nauli lakini ikishukishwa hawapunguzi nauli. Huu ni unafiki unaofaa kukomezwa kabisa," alisema Mzee Aba, mmoja wa wasafiri.

Wasafiri hao sasa wanaitaka serikali kupitia wizara ya uchukuzi kuunda sheria itakayo dhibiti utozaji wa nauli, na kuwalazimu wenye magari kupunguza nauli kulingana na bei za mafuta.

Siku ya Jumapili, tume ya kudhibiti kawi nchini ERC ilitangaza bei mpya za mafuta nchini ambapo mafuta ya dizeli ilishuka kwa shilingi 8.82, Petroli shilingi 2.14 huku mafuta taa ikishuka kwa shilingi 6.51.

Hii ni mara ya tano chini ya mwaka mmoja kwa tume hiyo kutangaza kushuka kwa bei ya mafuta, ambapo bei hizo mpya zilitarajiwa kuanza kutekelezwa usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu.