Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa wadi ya Tabaka eneo bunge la Mugirango kusini Kaunti ya Kisii wamewateketeza washukiwa wawili wa mauaji ya mfanyibiashara mmoja wa eneo hilo la Tabaka.

Kisa hicho kilitokea baada ya mfanyibiashara mmoja kuawa kwa njia ya kutatanisha, ndiposa wenyeji hao wakaamua kuchukua sheria mikononi mwao na kuwateketeza wawili hao kutoka eneo hilo, huku washukiwa wengine wakinusurika kifo kwa kutorokea mafichoni.

Hata hivyo, nyumba za washukiwa wengine waliotoroka ziliteketezwa, huku hali ya usalama ikirejea baada ya maafisa wa polisi kutoka kituo cha Gesonso kuimarisha usalama ingawaje hasara kubwa ilisababishwa.

Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumanne,  chifu wa lokesheni ya Tabaka Isaiah Mekenye alisema ilikuwa siku ya mauti katika eneo hilo kutokana na kisa hicho.

Kulingana naye, washukiwa walioteketezwa hawajajulikana kama walikuwa wahusika wa mauaji ya mfanyibiashara huyo au la, huku ikimlazimu chifu huyo kuitisha mkutano wa usalama ili jambo hilo kuzungumziwa kabla ya mauti kutekelezwa.

“Naomba watu kutochukua sheria mikononi mwao, na kisa ambacho tumeshuhudia leo ni kibaya sana,” alisema Mekenye.

Miili ya walioteketezwa inahifadhiwa katika chumba cha kuifadhi maiti cha Keroka uchunguzi unapoendelea.