Wasichana wanne wanaokabiliwa na madai ya ugaidi wametilia shaka ushahidi wa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mshtaka ya umma unaowahusisha na uvamizi wa chuo kikuu cha Garissa.
Kupitia wakili wao Hamisi Mwadzogo, washukiwa hao walionyesha kughadhabishwa jinsi wanavyohusishwa na uvamizi huo, ikizingatiwa walikuwa wameshakamatwa na kushitakiwa kwa tuhuma za ugadi kabla ya tukio hilo la Garissa.
Wakili Mwadzogo aliambia mahakama siku ya Jumatanano kuwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ina njama ya kukandamiza haki na uhuru wa wateja wake bila sababu mwafaka.
Aidha, aliongeza kuwa kwanini hadi sasa uchunguzi wa kesi hiyo bado kukamilika, ili haki na usawa kupatikana kwa wateja wake.
Vilevile, alipuuza madai ya naibu mkrugenzi wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti kuwa wateja wake wana uhusiano wa kigaidi na mataifa ya nje kama vile Uingereza, nchi za Jumuiya ya kiarabu, Uturuki na Sudan, na kuitaja hatua hiyo kama njama ya kuwakandamiza.
Haya yanajiri baada ya afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma kuwasilisha ombi katika mahakama kuu la kufutiliwa mbali dhamana iliyopewa wasichana hao.
Wasichana hao walikamatwa katika eneo la El-wak, lililoko karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, kaunti ya Garissa wakiwa safarini ikiaminika walikuwa wakieleka nchini Somalia kujiunga na kundi la Al shabaab.
Watatu hao Ummulkheir Abdullah kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 21, Mariam Said Aboud pamoja na Khadija Abubakar wenye umri wa miaka 19 wote kutoka Malindi wanadaiwa kuwa wanafunzi walioahidiwa ufadhili wa kimasomo, huku Halima Aden akikamatwa katika kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi.