Maafisa wa polisi katika kaunti ya Nakuru, Jumatatu waliwatia mbaroni washukiwa wanne wanaohusishwa na uvaamizi uliotekelezwa na makundi mawili ya kihalifu yanayozozana katika mtaa wa Flamingo viungani mwa mji wa Nakuru siku chache zilizopita.
Aidha msako huo ulisababisha kupatikana kwa lita 80 za pombe haramu ya kangara, lita 40 za busaa na bhangi zaidi ya kilo mbili.
Katika msako huo ulioongozwa na afisa anayesimamia polisi wa utawala AP katika kaunti ya Nakuru Barnabas Kimutai, maafisa hao pia walipata kadi za simu ambazo washukiwa hao hutumia kulaghai watu wasio na ufahamu.
“Tulianzisha msako asubuhi katika maeneo ya Mchanga na Kivumbini, ambapo tumenasa washukiwa wanne, bangi kilo mbili, busaa lita 40 na Kangara lita 80. Katika msako mwingine pia tulikuwa tumepata mapipa kumi ya pombe haramu,” Kimutai alisema.
Kulingana na Kimutai, wanne hao ni sehemu ya majambazi sugu ambao wamekuwa wakihusika na uporaji na uvaamizi dhidi ya raia.
“Tungetaka raia pia wajitokeze watupashe habari kuhusu magenge hayo ili nasi tukamate wanachama wake wote,” Kimutai aliongeza.