Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idadi ya wasichana ambao wanaavya mimba katika kaunti ya Uasin-Gishu na Bonde la Ufa kwa jumla inazidi kuongezeka.

Baraza la kitaifa la idadi ya watu na maendeleo limesema idadi kubwa ya wasichana husika ni wale ambao wako na umri wa kati ya miaka 15- 25.

Mshirikishi wa baraza hilo eneo la Bonde la Ufa Moses Ouma siku ya Alhamisi alisema hali hii ni changamoto kwa kampeni ya serikali ya kuhamasisha wakenya kuhusu umuhimu wa kupanga uzazi.

“Hali hii ni changamoto kwa juhudi za serikali za kuhamasisha wakenya kuhusu umuhimu wa kupanga uzazi, wengi wa wasichana hawa wanatoka katika familia maskini ambapo huwa hata vigumu kwao kulea watoto husika,” alisema Ouma.

Ouma aliongezea kuwa shirika lake linashirikiana na wadau wengine kuimarisha kampeini za uhamasisho miongoni mwa vijana ili kufikia chipukizi wengi na elimu kuhusu athari za mimba za mapema mbali na kupuuza wito wa serikali wa kupanga uzazi.

Akihutubu mjini Eldoret wakati wa kongamano kwa wanahabari kuhusiana na maswala ya kupanga uzazi, Ouma alitaka wakenya wa matabaka yote kukumbatia mpango wa uzazi ili kuchangia katika maazimio ya ruwaza ya 2030.

Hata hivyo hivyo, afisa huyo amekosoa wanaume ambao hupuuza mpango wa uzazi katika familia zao.

“Ni kweli wanaume wengi wamepuuza uhamasisho wa kushiriki vilivyo katika mpango wa uzazi, wanaume wengi wamechukulia mpango wa uzazi kama wa wanawake tu ambapo hata wanawake wenyewe hawapewi nafasi ya kupanga uzazi,” alisema Ouma.

Ouma aidha alisema serikali haina nia ya kulazimisha wakenya kupanga uzazi, bali inawataka wawe na watoto ambao watamudu kuwalea.