Hali ya wasiwasi imeendelea kuzingira eneo la Maela mjini Naivasha baada ya zaidi ya wakazi elfu moja kuvamia ardhi za kibinafsi na kuanza kuzigawa.
Wakazi hao mapema Jumatatu walivamia ardhi hizo zinazoaminika kumilikiwa na wakurugenzi wa shamba la Ng’ati huku uongozi kuhusu usimamizi wa ardhi hiyo ukiendelea kutokota.
Hatua hiyo aidha imejiri wiki moja baada ya vijana wengi kuvamia ardhi hizo na kuharibu mali ya dhamani kubwa.
Mwakilishi wadi wa eneo hilo Kariuki Mujing’a amedhibitisha hali hiyo na kusema kuwa wakurugenzi hao hawakuwa wamegawa ardhi hiyo vilivyo tukio ambalo limewagadhabisha wakazi hao.
“Shida hii ilianza wakati wakurugenzi hawa walipoongezea idadi ya wale watakaobahatika na ardhi hii kutoka watu 581 inayojulikana mpaka 830 kwa sasa,” Mujing’a aliongeza.
Aidha kiongozi huyo amesema kuwa wanataka majibu kutoka kwa wakurugenzi hao ili kujua jinsi ekari 3, 093 zilivyouzwa kwa shirika la KenGen huku kila mwanachama akipata shilingi 415, 000.