Hali ya wasiwsi ilitanda Alhamisi katika shamba la Ngongongeri kwenye mpaka wa kaunti ndogo za Njoro na Molo mjini Nakuru kufutia shambulizi la mchana lililoibuliwa kati ya kundi linalodaiwa kufadhiliwa na kiongozi mmoja wa zamani kwenye utawala wa KANU na wanachama wa jamii ya Ogiek.
Tatizo lilianza saa nne mchana wa Alhamisi wakati kundi hilo ambalo lilikuwa limejihami kwa nyuta na mishale lilidaiwa kuwafurusha watu waliokuwa wakivuna viazi kwenye mashamba yao.
Hali hiyo ilifanya wakulima hao kukimbilia usalama wao, huku nao vijana wa jamii ya Ogiek wakijihami kukabiliana nao.
“Hao watu walikuwa zaidi ya sitini, na tulipowauliza kuna nini, hawakutaka kutujibu ila walituelekezea silaha jambo lililotulazimu kukimbia. Sisi kama jamii ya Ongiek, hatupigani na wenzetu kutoka Tugen, tunapigana na matajiri, ambao ndio wameajiri wahuni hawa,” Simon Ndembere alisema.
Hata hivyo polisi waliingilia kati haraka na pamoja na watawala wa mkoa eneo hilo, wakafanya mkutano na makundi hayo mawili.
Naibu kaunti kamishna wa Njoro Peter Kinyanjui na mwenzake wa Molo Judith Cheruiyot walioongoza mkutano huo pamoja na kamanda wa polisi tawala eneo la Njoro Adan Mohammed, walionya makundi hayo mawili dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao.
Kinyanjui aliwataka wakaazi kutulia hadi tatizo hilo litatuliwe na tume ya ardhi nchini NLC, ambayo imetoa makataa ya siku 21.
“Uchochezi unatoka pande zote mbili, na hapa nataka kuwahakikishia kwamba tutakamata wachochezi wote, na hatutabembeleza yeyote ati kwa sababu ni mkubwa ama ana pesa. Vita tuache, na mfahamu hakuna aliye juu ya sheria,” Kinyajui alisema.
Majuma kadhaa yaliyopita mwenyekiti wa NLC Mohammed Swazuri akizungumza katika shamba la Barina kaunti ndogo ya Rongai alisema kaunti ya Nakuru ndiyo inaongoza katika mizozo ya mshamba kitaifa.