Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi ya Christ the King iliyoko mjini Nakuru, Niceta Munyi amewahimiza watahiniwa wa mtihani wa darasa la nane wa KCPE kutotumia njia za udanganyifu wanapofanya mitihani hiyo.
Kwenye mahojiano na mwanahabari huyu mjini Nakuru siku ya Jumatatu, mwalimu huyo aliwataka watahiniwa kuzingatia kanuni za mtihani huo.
“Siku ya Alhamisi wiki jana tulikuwa kwenye mkutano ambapo walimu wakuu walifahamishwa kuhusiana na jinsi mitihani ya kitaifa itaendelezwa. Pia tulijadiliana kuhusu udanganyifu kwenye mitihani na tukaonywa kuhusiana na utumizi wa simu za rununu katika mitihani,” alisema Munyi.
Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi ya St Joseph Geofrey Machoka, iliyoko mjini Nakuru alisema kuwa anatumai shule yake itapata kupata matokeo bora.
Aidha, alisema kwamba mambo yote yako shwari akiongeza kwamba wasimamizi wameeleza watahiniwa kuhusiana na kanuni na sheria za mtihani huo ili kuhakikisha hakuna dosari.
Wakati huo huo, alisema kuwa mgomo uliokuwa umetishia kuvuruga mitihani ya kitaifa hautakuwa na athari yeyote kwa watahiniwa na hautaadhiri matokeo ya mtihani huo.
“Tumepokea wasimamizi wa mitihani hiyo ambao wamezungumza na watahiniwa na nina uhakika kwamba wanafunzi hawa wako tayari kwa mitihani hiyo,” alisema Machoka.
Kwa upande wao, watahiniwa walisema kuwa wana imani kuwa watafanya vyema na kuzua alama bora.