Watalii wa kigeni wameitaka wizara ya uchukuzi kutoa nafasi kwa kampuni za kibinafsi kuanzisha huduma za kuvukisha abiria katika kivuko cha feri ili kupunguza msongamano wa abiria na magari.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu katika ufuo wa Florida, watalii hao waliitaja hatua hii kama bora zaidi kwani italeta ushindani wa kibiashara kati ya kampuni hizo na shirika la feri, hivyo basi huduma bora kutolewa kwa abiria wote.
Wakiongozwa na Adalwolf Adelberto kutoka Ujerumani, watalii hao walionyesha kughadhabishwa jinsi muda mwingi hupotezwa katika kusubiri feri kuwavukisha abiria kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Adelberto alisisitiza kuwa shirika hilo linafaa kuweka kiwango maalum cha abiria watakao ingia ndani ya feri, kinyume na inavyofanyika kwa sasa, ili kuepuka kuzama kwa feri hizo ili kuepuka maafa yasitokee.
Itakumbukwa wiki chache zilizopita shirika hilo lilikumbwa na matatizo, hasa baadhi ya feri kuharibika na kutatiza uchukuzi katika sehemu hiyo ambayo ilipelekea mkanyagano wa abiria.