Share news tips with us here at Hivisasa

Watu watatu wanauguza majeraha kufuatia ghasia zinazoshuhudiwa katika eneo la Kosovo huko Naivasha kufuatia mzozo baina ya jamii zinazoishi sehemu hiyo.

Polisi zaidi wametumwa eneo hilo linalopakana na msitu wa Eburu ili kutia kikomo kwa mzozo baina ya jamii ya Masaai na jamii nyingine zilizoko sehemu hiyo.

Watatu hao wanauguza majeraha ya mkuki huku mmoja akipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Rift Valley.

Naibu kamshna eneo la Naivasha Abraham Kemboi amesema kamati ya usalama ilikuwa imeshiriki mikutano kadhaa ya amani na viongozi wa sehemu hiyo ili kupata suluhu.

“Awali kamati ya usalama ilikuwa katika mkutano katika eneo hili na tuliweza kujaribu kusuluhisha mizozo ambayo tumekuwa tukishuhudia katika eneo hili, ni matumaini yetu kuwa mambo yatatulia na nawahimiza jamii zinazozozana ziweze kutulia na kuishi kwa amani,” alisema Bw Kemboi.