Dereva mmoja wa gari la kubeba mizigo anauguza majeraha katika hospitali moja mjini Naivasha baada ya kutekwa nyara na genge la majambazi kwenye barabara kuu ya Nakuru kuelekea Naivasha.
Wezi hao walimfungia dereva huyo kwenye msitu mmoja eneo la Marula baada ya kumpatiliza kichapo kikali na kumpora pesa zake zote, na hatimaye wakatoroka na gari hilo.
Hata hivyo dereva huyo aliweza kujiokoa na kuripoti tukio hilo kwa polisi ambao walianzisha msako wa wezi hao.
Aidha genge hilo halikuwa na bahati kwani walipokuwa wakitoroka waliingia kwenye barabara ya Kaskazini mwa ziwa la Naivasha kabla ya gari hilo kubingiria mara kadhaa eneo la Eburru, huku wezi hao wakitoroka na majeraha.
Maafisa wa polisi mjini Naivasha wameanzisha msako dhidi ya wezi hao na kuwataka wakaazi wa sehemu hiyo kuripoti mtu yeyote atakayepatikana na majeraha.