Watoto wawili mapacha wenye umri wa mwaka mmoja unusu wameokolewa na polisi baada ya kufungiwa nyumbani kwa siku tatu bila chakula na mama yao katika eneo la Maweni huko Ukunda.
Watoto hao wamepatikana wakila kinyesi chao ndani ya nyumba walimokuwa wamefungiwa na mama yao, anayeaminika kujihusisha na biashara ya ukahaba.
Majirani wamemtuhumu mama huyo kwa kuwatelekeza watoto wake, na kudai kuwa muda mwingi amekuwa akiutumia kwa kujihusisha ma maswala ya ukahaba na unywaji wa pombe na kuwanyima wanawe hata chakula.
Mama huyo aidha amejitetea kwa kumnyoshea kidole cha lawama mumewe aliyekuwa akiishi naye kwa masaibu yake.
Afisa mkuu wa polisi eneo la Msambweni Joseph Omijah amethibitisha kisa hicho na kutoa onyo kali kwa wazazi watakaopatikana wakitelekeza wanawao kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa sasa mwanamke huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Diani na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka ya kuwatelekeza watoto wake.