Zaidi ya wahasiriwa 300 ambao walifurushwa kutoka katika misitu ya Koromat na Nabkoi katika kaunti ya Uasin Gishu walishiriki maandamano kulalamikia kutengwa katika fidia.
Wahasiriwa hao walitaka serikali iwalipe fidia kama walivyoahidiwa walipokuwa wakifurushwa kutoka katika misitu husika.
Kulingana na viongozi wa wahasiriwa hao ni kwamba kuna njama ya kuwatenga kabisa katika mpango wa kuwapa makao mbadala.
Wakati wa maandamano hayo shughuli katika barabara kuu ya Eldoret –Nakuru karibu na kituo cha biashara cha Kondoo Burnt Forest zilisitishwa kwa muda.
Wahasiriwa hao wanadai kutengwa katika mpango huo huku mgao wao ukipewa watu ambao si wahasiriwa.
Mwenyekiti wa kundi hilo bw George Kimtai alidai kuwa utawala wa eneo hilo umekataa kuwapa usaidizi unaostahili kutafuta haki yao.
“Tunashangaa kila wakati tunapoenda kwa afisi ya chifu kutoa malalamiko yetu chifu anatufukuza huku akisema kuwa hakuna fidia ambayo tutapewa” alisema Bw Kimtai
Kimutai alidai kuwa fedha ambazo kundii lake lilipaswa kupewa zimepewa watu kutoka kaunti jirani za Nakuru,Elgeyo/Marakwet,Nandi miongoni mwa kaunti nyingine.
Kilio chao kiliungwa mkono na mbunge wa Kesses Bw James Bett ambaye alitaka serikali kuheshimu ahadi ya kwapa makao mbadala wahusika huku, akikiri kuwa ufisadi umeingizwa katika mpango huo.
Bett alisema tayari amewasilisha kilio cha watu hao kwa idara husika huku akitoa ahadi kwamba atatumia kila mbinu ili kuona kwamba wahasiriwa wamepata haki yao.
Pia alionya baadhi ya viongozi wa serikali dhidi ya kuingiza ufisadi katika swala hilo.