Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Watu wasiopungua 10 wanapokea matibabu katika hospitali ya KITI, na zingine zilizo karibu, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani karibu na taasisi ya masomo ya KITI, eneo bunge la Bahati.

Gari lilikuwa likitoka Maili Sita kuelekea Nakuru mjini Jumatatu, wakati liligonga mti na kusababishia abiria hao majeraha madogo madogo.

Wasamaria wema ambao walikuwa karibu waliharakisha kuokoa abiria hao na kuwakimbiza katika hospitali zilizo karibu kwa matibabu. Iliarifiwa matatu hiyo haina kibali cha kuhudumu kwenye barabara hiyo, na dereva na utingo wake walitoroka baada ya ajali.

Sasa abiria wanaitaka mamlaka ya usafiri na usalama barabarani NTSA pamoja na mamlaka ya ukarabati wa barabara kuu nchini KenHA, kushirikiana kumwajibisha mwanakandarasi aliyekarabati barabara ya Nakuru Subukia, kati ya eneo la Section 58 na Maili Kumi.

Wasafiri kwenye barabara hiyo wamekuwa wakiteta vikali kutokana na ubovu kwenye barabara hiyo.

“Gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi kwa sababu pahali hapa hakuna matuta kama sehemu zingine za barabara hii,” Paul Munyua, aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema.