Watu wanne waendelea kupata matibabu katika hospitali ya Matuu level five baada ya kushambuliwa na nyuki siku ya Jumapili katika eneo la Msingini, kaunti ndogo ya Yatta.
Akidhibitisha kisa hiki mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda katika eneo hilo Joshua Muli, alisema kuwa walioshambuliwa ni watoto wawili, mwanamume mmoja na ajuza mmoja aiyekuwa akimwokoa mjukuu wake.
"Watoto hao wawili walikuwa wakitoka kanisani waliposhambuliwa ghafla na nyuki wasiojulikana walikotoka kisha mwanamume huyo na ajuza wakaja kuwaokoa watoto wale waliolia kwa kuchanganyikiwa wasijue cha kufanya," alisema Muli.
Aidha wakaazi eneo la Kwangii wamelitaka shirika la Wanyama pori nchini (KWS) kuingilia kati na kuwanusuru kutokana na kiboko pamoja na ndama wake ambao wamekuwa wakiharibu chakula shambani na pia kuwauwa mifugo yao.
Kulingana na wakaazi hawa kiboko huyu na ndama wake huvamia mashamba yao nyakati za usiku.
Morris Mbuvi mmoja wa wakaazi alielezea jinsi alivyoamka asubuhi na kumkuta ng'ombe wake amekufia zizini baada ya kuumwa na kiboko.
Vilevile alisema kuwa mbuzi wa jirani wake alikatanishwa kuwili na kiboko huyu na kwa sasa wakaazi wanaishi kwa hofu kushambuliwa na mnyama huyu hasaa wanao.
"Kando na kuharibu mimea na kuua mifugo yetu tuna hofu ya kushambuliwa na mnyama huyu," alielezea Mbuvi.