Wakazi mjini Naivasha waliamkia mshangao Ijumaa asubuhi baada ya kupata miili ya watu wawili waliouawa na kutupwa barabarani.
Katika kisa cha kwanza, wakazi wa eneo la Kihoto walipata mwili wa mfanyikazi mmoja wa kampuni ya maua mjini humo ukiwa umetupwa kando ya barabara ya Naivasha kwenda Mai Mahiu.
Haikubainika ni vipi mwanaume huyo aliuawa wala waliohusika kwani wakazi walipata mwili wake ukivuja damu kichwani.
Katika kisa cha pili, mfanyibiashara mmoja mwenye umri wa miaka 30 alipatikana ameuawa eneo la Karagita huku mwili wake ukiwa na ishara ya kudungwa kwa kisu mara kadhaa.
OCPD wa Naivasha Titus Munyoki alithibitisha visa hivyo na kusema kuwa uchunguzi unaendeshwa kubaini waliohusika.
Munyoki aliwasihi wakazi kutoa habari zitakazosaidia kutiwa mbaroni kwa waliotekeleza mauaji hayo.
"Tunawaomba ikiwa mtu yeyote atakuwa na habari muhimu kuhusu mauaji haya asisite kuwasilisha ripoti kwa polisi," Munyoki alisema.
Wakaazi wa Naivasha wameteta kuwa visa vya uhalifu vimekuwa vikiongezeka kwenye mitaa ya mji huo haswa wakati huu wa msimu wa krisimasi.