Waumini wa kanisa la Repentance and Holiness Ministry kutoka maeneo mbali mbali ya taifa wanaendelea kumiminika jijini Kisumu mbele ya mkutano wa maombi ya kufunga mwaka 2015 na kufungua mwaka 2016.
Kulingana na mhubiri wa kanisa hilo Hellen Ochieng, tayari maandalizi ya mkutano huo yamekamilika.
“Maandalizii yote mbele ya mkutano huo yamekamilika, na kinachoendelea kwa sasa ni kuhimiza kila mmoja kujitokeza kuhudhuria mkutano huo ili kupokea muujiza wake,” alisema mchungaji Ochieng.
Mkutano huo mkubwa wa injili, utaongozwa na Nabii Edward David Owour wa kanisa la Repentance and Holiness Ministry, katika uwanja wa Kibos jijini Kisumu kuanzia tarehe 30 mwezi huu, hadi mkesha wa kuamkia tarehe moja mwezi Januari.
Baada ya hapo, Nabii Owuor ataongoza kongamano la wahubiri katika uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Kisumu tarehe mbili mwezi Januari.
Usalama umeimarishwa vilivyo, ikizingatiwa kuwa watu kutoka maeneo mbali mbali nchini na hata ulimwenguni watahudhuria.
Awali, mkuu wa usalama wa eneo la Nyanza Francis Mutie alisema kuwa vikosi vya usalama vitakuwa chonjo wakati wote wa mkutano huo.
Mutie alisema kuwa watazingatia kuomba maafisa zaidi wa usalama kutoka kaunti jirani, ili kuimarisha usalama hata zaidi, iwapo kutakua na haja ya kufanya hivyo.