Tarehe 14 Februari, ni siku inayosherehekewa duniani kote kama siku ya wapendanao maarufu kama Valentines Day.
Hata hivyo wafanyibiashara wa kuuza maua mjini Mombasa wanasema biashara imeshuka wakati wa msimu wa Valentines mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Wafanyibiashara hao wamesema walitegemea kupokea wateja wengi wakati huu ambapo shamrashamra za sherehe za Valentines zimeanza kabla siku yenyewe.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika duka lake mjini humo, Mohamed Ruwa alisema kuwa hali ya wateja kuadimika wakati kama huu inatwatia wasiwasi.
“Miaka ya nyuma ilikuwa mwezi Februari ukiingia tu wateja wanaanza kumiminika lakini sasa hivi naona siku inakaribia lakini duka limekauka wateja,” Alisema Ruwa.
Hata hivyo Ruwa anayemiliki duka la Petals Florist anataja gharama ya juu ya maisha kama chanzo cha kutokea kwa hali hiyo.
“Sababu halisi siwezi nikajua lakini kwa kukisia tu mimi nadhani ni ugumu wa maisha kwa sababu pia ukiangalia mwezi Januari ndio huo umekamilika nna watu wengi wametumia pesa sana,” aliongeza Ruwa.
Hata hivyo wafanyibiashara wengine wanasema kuwa hali hiyo ilianza kushuhudia tangu mwezi Disemba mwaka jana ambapo wengi wao walitarajia wateja kuja kununua mauwa kwa ajili ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Wakati huu wa msimu wa Valentines watu wengi humiminika katika maduka ya kuuza zawadi mbalimbali huku zawadi inayonunuliwa zaidi ikia ni maua kuashiria mapenzi.
Mbali na kuuza maua, wafanyibiashara pia wanatarajia kuuza bidhaa mbalimbali siku ikiwa ni chakula, mavazi pamoja na huduma zingine.