Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Polisi wa kuzima ghasia walitibua jaribio la kikundi kimoja cha wafanyibiashara kuandamana Jumanne mjini Naivasha, kupinga hatua ya serikali ya kaunti ya Nakuru kuongezea ada zinazotozwa wasafirishaji wa mchanga wa ujenzi eneo la Mai Mahiu.

Polisi hao waliendelea kukita kambi eneo hilo huku wafanyibiashara hao wakiapa kutoendeleza shuguli za usafirishaji wa bidhaa hiyo muhimu ikiwa malipo hayo mapya hayatatupiliwa mbali.

Mmoja wao, Moses Wachira, amesema kuwa serikali ya gavana Kinuthia Mbugua ilitoa ilani ya kuongezea ada hizo wiki jana kwa kila lori linalosafirisha mchanga huo.

“Kwa sasa tunatakiwa kutoa shilingi elfu moja kwa lori ndogo, na hapo mbeleni tulikuwa tunatoa mia nne. Lori kubwa sasa linatozwa hadi shilingi 2,500 kutoka kwa shilingi elfu moja, na tunaona hii ni dhulma kwetu,” alisema Wachira.

Naye Hilary Wambugu, mwanabiashara mwingine amesema serikali hiyo ya kaunti inawaongezea ada hizo kiholela, licha ya kuzembea kukarabati barabara za maeneo hayo.

Polisi wamesema kuwa usafiri haukusitishwa kwa njia yeyote kwenye barabara ya Naivasha kuelekea Mai Mahiu na Mahiu kuelekea Narok ambako watu hao walikuwa wakipania kufanya maandamano yao.