Wawakilishi wa bunge la kaunti ya Nyamira wanataka bunge hilo kununuliwa na kuwekwa vipasa sauti vya kisasa ili kuepukana aibu wanayokumbana nayo wakati wanatembelea bunge zingine haswa bunge kuu na ile ya seneti ambazo zimewekwa vipasa sauti vya kisasa mbele ya viti bungeni.
Kulingana na Mwakilishi wadi ya Rigoma Benson Sironga, walipata aibu wakati wa ziara yao ya hivi karibuni kwa bunge la seneti wakati walishindwa kuvitumia vipasa sauti vya kisasa vilivyokuwa kwenye bunge hilo.
“Iliwabidi wafanyikazi wa bunge hilo kuingilia kati na kutuonyesha jinsi ya kuvitumia vipasa sauti hali ambayo ilitusababishia aibu sana,” alisema Sironga
Sironga aidha alisema kuwa itakuwa vyema iwapo vipasa sauti hivyo vitanunuliwa na kuwekwa kwenye bunge hilo, na akataka kujua mda utakaochukuliwa kwa mpango huo kuwasilishwa.
Aidha, kiongozi wa walio wengi kwenye bunge hilo na ambaye ni mwakilishi wa wadi ya Nyamaiya Laban Masira alisema kuwa wiki hii atawasilisha ripoti kamili bungeni kuhusu mipango ambayo bunge hilo itatekeleza haswa kuhusu swala hilo la vipasa sauti vya kisasa.
“Ninajua bunge letu lina changamoto mbalimbali, haswa ukosefu wa vipasa sauti na kuna mipango ya kuvinunua,” alisema Masira.