Mwakilishi wa wadi ya Bokimonge Kaunti ya Kisii George Bibao amewaomba wawakilishi wa wadi katika kaunti hiyo kuungana pamoja ili kutembelea miradi ya maendeleo ambayo imefanywa na serikali ya kaunti hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya wawakilishi hao kurefusha vikao vyao na kusema wakati huu ndio mwafaka kutembelea miradi ya maendeleo katika wadi za kaunti hiyo ili kuonyesha uwazi kwa wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla.
Kulingana na mwakilishi huyo, ripoti ambayo ilitolewa na serikali ya kaunti hiyo inaonyesha kuwa miradi mingi tayari imefanywa katika wadi za kaunti hiyo, jambo ambalo mwakilishi huyo anadai la uongo na kuomba wawakilishi wote kutembelea wadi ili kubaini yaliyoandikwa kwa ripoti na kuona yale yametekelezwa .
Kulingana na miradi ambayo serikali hiyo imefanya ni ukarabati wa barabara nyingi, ukarabati wa soko, zahanati, maji, miongoni mwa miradi mingine ambayo mwakilishi huyo anadai itembelewe kabla ya kuenda likizo ya Desemba.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, Bibao alisema hawezi kuamini jinsi pesa za serikali hiyo zilitumika kwani ripoti inaonyesha miradi mingi imefanywa, jambo ambalo haliambatani na tathimini yake katika wadi yake na wadi zingine.
“Naomba wawakilishi wa wadi tuungane tuanze kutembelea miradi ile inadaiwa kufanywa na pesa tayari kulipwa ili tujue jinsi pesa za maendeleo zimefanya kazi,” alisema Bibao.
Matamshi ya mwakilishi huyo yaliungwa mkono na mwakilishi wa Boikang’a Elkanah Nyandoro kwa kusema sharti uwazi uonekane kwa pesa za umma kwa kuwajibika kwa maendeleo.